UKAME WAGEUZA MAEMBE KUWA MLO KWA BAADHI YA FAMILIA SENGEREMA.




Na, Paulina  Mpiwa, Sengerema Mwanza.

Baadhi ya wananchi wa mtaa wa Mwabayanda  uliopo katika kijiji cha Kizugwangoma   Kata ya Misheni   Wilayani Sengerema  mkoani Mwanza wamelazimika kula mlo mmoja huku  wengine wakishindia  maembe kutokana na  kukosa  chakula.

Wamesema  licha ya kujitahidi kulima eneo kubwa  la  mazao  mbalimbali   ikiwemo  mahindi lakini yamenyauka kwa jua kwa sababu ya ukame uliokumba maeneo  mengi  ya nchi. 

Kufuatia hali ya ukosefu wa chakula  wananchi   hao  wameiomba  Serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia chakula  cha msaada ili  kunusuru ukata huo.

Kutokana  na  hali hiyo Mulika jamii imemtafuta Mkuu wa wilaya ya Sengerema Bwn,Emmanuel  Kipole  kuzungumzia suala hili ambapo amesema serikali ya awamu ya tano   imekwisha  toa maelekezo  kuwa haitatoa  chakula na badala yake wananchi waendelee kuwa na matumaini  huenda mvua zitaendelea kunyeza na kusisitiza wapande mazao yanayostahimili ukame .   

Hata hivyo Agosti   10  ,2016       Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt,John Pombe Magufuli  akihutubia mamaia ya  wananchi wa  Sengerema   katika uwanja wa mnadani alisema serikali ya awamu ya tano haitakuwa na huruma ya kutoa chakula kwa watu wanaokichezea.

Awali mamlaka ya hali ya hewa nchini ilitoa taarifa  ya uwepo wa mvua za wastani katika maeneo mengi ya nchi na kutoa ushauri kwa wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo kwa kulima mazao yanayokomaa muda mfupi na yanayostahimili ukame ili kuepukana na baa la njaa.


TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 Response to "UKAME WAGEUZA MAEMBE KUWA MLO KWA BAADHI YA FAMILIA SENGEREMA."

Post a Comment