RADIO JAMII TANZANIA ZATAKIWA KUPAZA SAUTI ZA WANYONGE.



Na, Paulina Mpiwa/Mary.


 Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeahidi kuendelea kuzisaidia redio jamii kwa lengo la kuhakikisha sauti za wanyonge zinapazwa na kusikika ili kukuza demokrasia nchini. 


Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA), jijini Dar es  salaam Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la UNESCO nchini Zulmira Rodrigues ,amesema wakati umefika kwa wadau wa sekta ya habari kufikiri kwa kina namna ya kuhabarisha umma kwa kuangalia namna ya uwasilishaji taarifa zao. 


Amesema kwa wanahabari wanapaswa kuwa makini na taarifa wazitoazo kwa jamii kwani kumekuwa na mazoea ya baadhi yao kuripoti habari bila kufanya uchunguzi wa kina huku wakitumia chanzo kimoja cha habari badala ya kujiuliza maswali mengi ili kupata taarifa sahihi. 


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya COMNETA, Mohamed Tibanyendera amesema kuwa kwa siku za nyuma redio ilikuwa ni chombo cha kuaminika katika utoaji wa habari hivyo kujijengea umaarufu na kuaminika zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna upotoshaji mkubwa. 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania-COMNETA, Prosper Kwigize ameeleza kuwa ipo changamoto kwa baadhi ya maafisa habari mikoani na wilayani kuleta urasimu mkubwa katika utoaji wa taarifa zinazohitajika kwa waandishi wa habari hivyo kukwamisha upatikanaji wa habri kwa umma. 

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 Response to "RADIO JAMII TANZANIA ZATAKIWA KUPAZA SAUTI ZA WANYONGE."

Post a Comment