Upungufu wa Vyumba vya Madarasa waleta Msongamano

Na Bernadetha Mwakilabi, Kongwa Dodoma

Shule ya msingi Hogoro iliyopo kata ya Hogoro wilayani Kongwa  inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo kutokana na msongamano wa wanafunzi shuleni hapo.

Hayo yameelezwa leo na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi Enesia  Mwigune wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo ameeleza kuwa shule yake inakabiliwa na upungufu wa vyumba 17 vya madarasa.

"hali ya vyumba vya madarasa katika shule yangu mahitaji ni 24 yaliyopo ni 7 na pungufu ni 17 kwahiyo hayakidhi mahitaji ya wanafunzi wangu ambao idadi yao ni 1,144" alisema Mwigune.

Mwigune alieleza changamoto nyingine iliyopo katika shule yake kuwa ni pamoja na upungufu wa matundu ya vyoo kwani mahitaji ya jumla ni matundu 52 lakini yaliyopo ni matundu 10 na pungufu ni 42 hivyo wanafunzi wapo katika mazingra magumu ya kiafya.

Mwigune alieleza kuwa changamoto hizo za upungufu wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo utazidi kuleta hali ngumu ya ufundishaji kwa mwaka 2017 kwani mpaka sasa uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali kwa mwaka 2016/2017 umefikia wanafunzi 154 ambapo kwa mwakani idadi ya wanafunzi itaongezeka.

Mwigune alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Bw Deogratius Ndejembi kwa kuliona tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule yake na hatua alizozichukua kwa kuhamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa.

"tunamshukuru mkuu wa wilaya kwa kuona uzito wa changamoto hii kwa kuhimiza wananchi kwani mpaka sasa wamechangia mifuko 40 ya saruji, matofali 1,300 na tayari hatua za awali za kuchimba msingi zimeanza " alisema Mwigune.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Bw Ndejembi aliahidi kutoa mifuko ya saruji itakayosalia hadi kukamilika kwa ujenzi wa vyumba hivyo vitatu vya madarasa na kuwataka wananchi wa Hogoro kuendelea na ujenzi huo mpaka mwisho kwani ni moja ya shughuli za maendeleo kijijini hapo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 Response to "Upungufu wa Vyumba vya Madarasa waleta Msongamano"

Post a Comment